fbpx

Jiwe La Nyoka Na Utapeli Mwengineo

Share on facebook
Share on google
Share on twitter
Share on linkedin
Share on pinterest

Kiufupi, Mawe ya nyoka au Jiwe la sumu ya nyoka au Jiwe jeusi, hayafanyi kazi hata kidogo, hasa tukiongelea kuondoa sumu kwenye eneo la mwili lililong’atwa na nyoka.

Dunia ina vituko vingi mno, na mara nyingi vituko hivi huweza kwenda miaka mingi, kizazi baada ya kizazi pasipo kujulikana na wengi kutojiuliza nini hasa kinachotokea. Vituko hivi vinaweza visiwe na madhara, lakini pale mtu anapojitungia “tiba” fulani haswa kwenye maswala ya dharura, ni wajibu wetu kama madaktari kujaribu kufumbua macho.

Kuanzia kumkojolea mtu ili kuzuia degedege, kumwagia maji aliyezimia  n.k na vitimbi vyengine nilivyosikia wagonjwa wakifanya toka nasomea udaktari mpaka leo hii, hebu tuangaze kuhusu haya “mawe yanayonyonya sumu ya nyoka” na kujua yanafanyaje kazi ili kuelewa kwa nini watu wengi (mpaka wenye elimu za juu) wanayaamini.

Nimechagua kuandika kuhusu hili kwa sababu mahala ninapoishi kunajulikana kuwa na nyoka wengi sana hivyo kila nyumba na familia huwa na mbinu walizojiwekea kukwepa nyoka hawa (ya kwangu ni kutotoka nje bila sababu za msingi).

Jinsi hesabu zinavyofanya kazi

Kati ya jamii ya nyoka zaidi ya 3000 duniani, karibu nyoka 600 tu wana sumu, na kati ya hao, ni chini ya nyoka mia mbili tu wana sumu inayoweza kuhatarisha maisha yako.

Kutokana na nyoka wengi walio na sumu na wasio na sumu kufanana, na watu wengi kuwa na elimu ndogo kuhusu nyoka (au kutojua kabisa) ni sawa kimahesabu kusema kuwa mawe haya hutumika zaidi kwa nyoka wasiokuwa na sumu kutokana na wingi wa nyoka hao.

Zaidi ya hapo hata nyoka waliokuwa na sumu hawatoi sumu muda wote wanapogonga (dry bites), inakadiriwa zaidi ya asilimia 20 ya majeraha ya nyoka ni nyoka kujilinda ambapo sumu haitolewi.

Hivyo ukiwa na watu watano ambao wameng’atwa na nyoka aliyethibitika kuwa mwenye sumu, mmoja wao “ataponyeshwa” na jiwe hilo kwa sababu hakuchomwa na sumu yeyote alipogongwa na nyoka. Umeelewa?

Hivyo ukichanganya hilo na idadi ya watu wote waliong’atwa na nyoka kisha kutumia mawe hayo, utaona jinsi gani ngano kama hizi zinavyoweza kushika kasi na huweza kuleta madhara makubwa kwa wale waliong’atwa na kuathirika na sumu kiukweli.

Yani leo hii nikichukua mizizi ya mchicha iliojiotea nyuma ya choo changu nikasema ni dawa ya kufyonza sumu ya nyoka, nitapata mashuhuda wengi sana na order nyingi ya dawa zangu, kwani mahesabu yananisongesha kwani wengi wataotumia hawatakuwa na sumu yeyote iliongia mwilini mwao.

Ni aina hii ya uhuni watu wanatumia kusema wanatibu saratani (kansa), utasa n.k. Kwani hata kama saratani inaua watu 95 kati ya 100 (asilimia 95) ndani ya miaka mitano (5-year survival rate), nikikaanga maua yangu nikanywesha watu mia, nategemea watu watano watapona ugonjwa huu, baada ya hapo nawaleta hao waliopona kutoa ushuhuda wa dawa yangu na wateja watazidi kumiminika. Huu ndio utapeli wa kimahesabu….. Sasa turudi tena kwenye nyoka…

Wanavyosema inafanya kazi

Jiwe la nyoka huwa ni kipande cha mfupa uliounguzwa ambacho huwekwa sehemu ilioumwa na nyoka na huganda hapo na kufyonza majimaji (wanayosema ni sumu) mpaka sumu yote itakapoisha kutoka kwenye kidonda kisha kubanduka na kudondoka ardhini na kimiujiza mgonjwa “hupona” (lakini ni uhuni).

Baada ya hapo jiwe hilo huchukuliwa kuchemshwa au kusafishwa na maziwa ili kuondoa sumu ili liwe tayari kwa matumizi mtu mwengine anapong’atwa na nyoka.

Linavyofanya kazi kiuhalisia

Mifupa (na mawe aina nyingi), una vitundu vidogo vidogo (highly porous) na ukiwekwa kwenye sehemu yenye unyevu unyevu hujishikiza na kufyonza maji ya sehemu ile kwa njia ya capillarity. Ni kama kamba ya taa ya chemli inavyofanya kazi (kwa wale tuliosoma na chemli) au hata tambara la kudekia.

Ukiweka tambara kavu kwenye sehemu yenye majimaji, hujishikiza na maji kuingia kwenye tambara hilo kwa kupitia vitundu hivi vidogo na maji hupanda juu mpaka tambara zima linajaa, hii ndio capillary action.

Mwishowe uzito wa majimaji hwenye ngozi huzidia jiwe hili na jiwe hudondoka chini, lakini uhalisia ni kwamba hakuna kiwango chochote cha sumu kilichoondolewa.

Vifaa vya kisasa vya “kuondoa sumu” (Uhuni wa kidigitali)

Vifaa vinavyodaiwa “kunyonya” sumu ya nyoka

Ukiangalia matangazo ya televisheni au mtandaoni, kuna vifaa “vipya” vya kuondoa sumu (Venom Extractors) na vinauzwa kwenye maduka makubwa nje ya nchi lakini uhalisia ni kwamba ni kama mawe ya nyoka yaliyoongezewa vifaa ili na sehemu ya kutunza na kuonyesha “sumu” hiyo ili vionekane kama vinafanya kazi haswa kwa watu wasiotafakari kwa kina.

“Extractor” hizi pamoja na mawe vyote ni kiini macho kwa kuonyesha vinaondoa damudamu na majimaji ya njano (ambayo hufanana na baadhi ya sumu za nyoka) kutoka sehemu mtu alipong’atwa lakini hii si kitu bali ni sehemu ya damu (serum) na majimaji mengineyo ambayo hutokea pindi uvimbe unapoanza sehemu yeyote ya mwili.

Kwa nini nasema vifaa hivi ni uzushi?

Kuna sababu nyingi kwa nini huduma hii ya kwanza haifanyi kazi, moja ni kuwa meno ya nyoka yamejikunja hivyo sehemu unapoona kwa nje alama za kung’atwa si kwamba sumu imeingia chini yake moja kwa moja (hii pia ni sababu kwa nini kuchana au kukata sehemu iliyoumwa na nyoka hakutofanya kazi).

Pili, Sumu ya nyoka baada ya kung’atwa huingia ndani kabisa (tissue compartments) na si tu chini ya ngozi  kisha sehemu meno yalipopita hujibana na kurudi mara tu baada ya kushambuliwa na nyoka.

Tatu, kiasi kikubwa sana cha sumu kinadhaniwa kuingia kwa kasi mno kwenye sehemu tofauti tofauti kwenye matabaka (tissues compartments). Hii ina maana hakuna njia ya moja kwa moja kati ya jeraha la nje na sumu iliyoingia ndani na kiasi kikubwa cha sumu tayari kimeshaanza safari yake.

Tafiti zinasemaje?

Katika tafiti za afya, maandiko yanayopewa kipaumbele ni yale yanayojumuisha tafiti nyingi kwa pamoja ili kufahamu ubora na uhakika wa taarifa, kitaalamu zinaitwa “systematic review studies” au “meta-analysis studies”

Katika Jarida la PLOS Neglected Tropical Diseases, Oktoba mwaka 2016 lilichapisha andiko liitwalo “Treatment of Snake bites in a First Aid Setting – A Systematic Review” ambalo lilichukua tafiti mbalimbali kwenye matibabu ya huduma ya kwanza ya mtu aliyeng’atwa na nyoka na kuangalia mbinu mbalimbali zilizotumika na matokeo ya mwisho ya matibabu (patient outcome).

Nitaangazia sehemu mbili tatu kwenye chapisho hili ili na baadhi ya tafiti walizotumia ili tuizike hii mada kiujumla, kwanza kwenye matumizi ya mawe ya sumu ya nyoka (snake stones), dawa za asili kutibu majeraha ya nyoka na tatu kunyoya “sumu” kutoka kwenye jeraha la nyoka (suction devices).

Tafiti kuhusu matumizi ya mawe ya nyoka

Utafiti wa Madaki et. al unasema

“There was no significantly decreased incidence of envenoming in snakebite victims using snake stones compared to those receiving no first aid”

Yani: “Hakuna tofauti yeyote ya msingi iliopo kati ya watu waliongatwa na nyoka kisha kutumia mawe na wale ambao hawakupewa huduma ya kwanza kabisa kwenye kupunguza sumu mwilini.”

Matumizi ya dawa za asili

Utafiti wa Madaki et. al pia unaongeza

 “The use of traditional medicine (both ingested and applied to the wound) in snakebite victims was not found to be significantly associated with a decreased occurrence of envenoming, compared to receiving no first aid.”

Yani: “Matumizi ya dawa za asili (za kumeza na kupaka kwenye jeraha) kwa watu waliong’atwa na nyoka hayakuleta tofauti yeyote muhimu katika kuondoa sumu ukilinganisha na kutopata huduma ya kwanza yeyote.”

Katika tafiti nyengineyo ilibaini:

“There was no significant difference in duration of hospital stay between snakebite victims treated with concoctions applied to the wound or ingested, compared to snake bite victims with no concoctions applied to the wound or ingested……. In contrast a significantly increased odds of death and disability was shown in snakebite victims with concoctions applied compared to snakebite victims with no concoctions applie to the bite wound.”

Michael et al.

Yani tafiti iliofanyika na Michael na wenziwe ilionyesha hakuna tofauti muhimu kwenye idadi ya siku za kulazwa hospitali kati ya watu waliotumia dawa za asili na ambazo hawajatumia, kisha akasema tofauti na hilo, watu waliotumia dawa za asili katika jeraha walikuwa kwenye hatari zaidi ya kifo na madhara  kuliko wale ambao hawakutumia dawa hizo.”

Kwa mtazamo wangu, watu waliotumia dawa za asili wanaweza kujipa imani ya kwamba wataponyeshwa na hiyo dawa na mwishowe kuchelewa kufika hospitali zaidi kupelekea vifo vyao, kuliko wale ambao hawakutumia “dawa” hizo na kuwahi kutafuta tiba sahihi.”

Kunyoya sumu kutoka kwene jeraha

Tafiti nyengine iliofanywa na Micheal et al. ilibaini:

 “There was no significant diference in outcome the occurrence of death, disability or amount of anti-venom required on use of a suction on a bite wound compared to no first aid.”

Yani: “Hakuna tofauti ya msingi katika matokeo, kifo, ulemavu au kiwango cha dawa kilichohitajika kwenye matibabu hospitalini (anti-venom) kwa wale waliotumia vifaa vya kunyonyea sumu (extractors n.k) ukilinganisha na wale ambao hawakupata huduma ya kwanza kabisa.”

Mwishowe tafiti hii ilishauri kuachana na vitimbi hivi asili katika huduma ya kwanza kwa muathitrika wa kugongwa na nyoka. Kiufupi, tafiti hazikubaliani na matumizi ya vitu hivi, na elimu ya afya inabidi iendeshwe kutokana na tafiti makini sio “bibi yangu alitumia likamsadia” ndio maana mimi natumia

Kumalizia

Huduma ya kwanza kwa aliyegongwa na nyoka ni jambo muhimu, na linahitaji kuongelewa kivyake katika mahala pengine. Matumizi ya mawe na vifaa vyengine vimepitwa na wakati na sisi kama wahudumu wa afya ni wajibu wetu kuifundisha jamii kuhusu mambo haya. Watu wengi hufanya hivi kwa nia nzuri na ni katika ubinadamu kusaidia wengine, lakini muda mwingi “msaada” wetu huweza kuwa na madhara zaidi kuliko faida.

Marejeo

  1. Avau B, Borra V, Vandekerckhove P, De Buck E (2016) The Treatment of Snake Bites in a First Aid Setting: A Systematic Review. PLoS Negl Trop Dis 10(10): e0005079.doi:10.1371/journal. pntd.0005079
  2. Madaki JKA, Obilom RE, Mandong BM (2005) Pattern of First-Aid Measures Used by Snake-bite Patients and Clinical Outcome at Zamko Comprehensive Health Centre, Langtang, Plateau State. Nig Med Pract 48: 10–13.
  3. Michael GC, Thacher TD, Shehu MI. The effect of pre-hospital care for venomous snake bite on outcome in Nigeria. Trans R Soc Trop Med Hyg 2011; 105: 95–101. doi: 10.1016/j.trstmh.2010.09.005 PMID: 21035155
Share on facebook
Share on google
Share on twitter
Share on linkedin
Share on pinterest

This Post Has 2 Comments

  1. nice treatise

    1. Thanks alot Fidel

Leave a Reply

Close Menu